Straika wa Yanga, Amissi Tambwe.
Hans Mloli na Khadija Mngwai
STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, ana mabao 14 katika Ligi Kuu Bara, sawa na Hamis Kiiza wa Simba, lakini amesema hatishiki na mtu yeyote katika vita ya kuwania kiatu cha dhahabu kwani anajua kazi yake.
Tambwe, raia wa Burundi, aliyewahi kucheza Simba kisha kutupiwa virago kama ilivyokuwa Kiiza, raia wa Uganda, aliyeichezea Yanga kisha kutupiwa virago, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, hana presha na kiatu cha dhahabu.
Hamis Kiiza.
Kauli hiyo ya Tambwe imekuja siku chache baada ya Kiiza kufunga mabao mawili dhidi ya Mgambo JKT na kufikisha mabao 14 huku Tambwe akifunga moja dhidi ya Prisons na kufikisha mabao 14, wote wapo sawa sasa.
Tambwe alisema: “Sina presha ya aina yoyote na wala sitishiki na kasi ya Kiiza katika ufungaji, najua amenifikia kwa mabao lakini mimi najua ninachofanya uwanjani, sipaswi kuwa na woga, nitafunga mpaka wengine wakasirike.
“Mchuano ni mgumu kuwania ufungaji bora kwani kila mtu anapambana, lakini ninachoangalia kwa sasa ni kuhakikisha najituma ipasavyo kumuacha mpinzani wangu.”
Straika huyo aliendelea: “Ligi ni ngumu sana, tena sana, kama hivyo unavyoona katika mzunguko huu wa pili kila timu imejipanga kuhakikisha inaonyesha uwezo wa hali ya juu na kufanya vyema, hivyo inatufanya kila mchezo kwetu kuwa fainali.
“Napambana na vitu viwili sasa, moja ni ushindi kwa timu na pili ni vita ya ufungaji bora katika ligi, kitu cha msingi ni kujituma mpaka mwisho ili niweze kufanikiwa na wala sina presha na mabao aliyofunga Kiiza.”
Gazeti hili liliwasiliana na Kiiza ambaye alisema: “Sijakitolea macho kiatu cha dhahabu zaidi ya kuipa ubingwa Simba, lakini hii haimaanishi nitaacha kupambana ili nifunge. Najua kuna vita kati yangu na Tambwe.
“Najua Tambwe atataka kufunga zaidi, nami nitafunga zaidi yake, mwisho wa siku tutakutana uwanjani kwani kila mtu yupo katika kikosi bora kinachoweza kumpa ufungaji bora.
“Ufungaji bora kwangu kama Simba haijatwaa ubingwa hauwezi kuwa mali, hivyo nitapambana ipasavyo na vita yangu na Tambwe haiwezi kuisha kirahisi kwani yeye atafunga na mimi nitafunga pia.”
Kiiza amecheza mechi 15 hivyo ana asilimia 93.3 ya ufungaji wakati Tambwe aliyecheza mechi 17 anazo 82.3%.
About Unknown
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 maoni:
Chapisha Maoni