MWENYEKITI WA YANGA, YUSUF MANJI |
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imetangaza Juni 05, 2016 kuwa siku ya Uchaguzi Mkuu wa viongozi ndani ya klabu ya Young Africans SC ya jijini Dar es salaam.
Uchaguzi huu ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu sana na wadau wengi wa soka, wengine wakiwa si wanachama wa Yanga.
Wengi wao waliamini uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Yusuf Manji na Makamu wake, Clement Sanga walikuwa wakiisigina katiba ya Yanga.
Manji alikuwa akisema, alikuwa akifanya kila linalowezekana kuusisitiza uchaguzi ufanyike lakini haikuwa hivyo.
Sasa uchaguzi umepangiwa siku, ujumbe wangu sasa ni kwa wale waliokuwa wakishinikiza chinichini wakidai uchaguzi.
Wako waliodai Manji analazimisha uchaguzi usifanyike na walinyimwa haki yao ya msingi. Huu ndiyo wakati mwafaka wa vitendo.
Huu ndiyo wakati mwafaka kuonyesha kweli waliihitaji demokrasia, wajitokeze na kugombea na wasiwe kama vyura. Kazi kupiga kelele wakisogelewa, wananyama kimya.
Isije ikawa ni kelele tu na fursa wameipata wakae kando. Kila mtu anajua Manji amefanya vizuri, lakini si vibaya Yanga kuwa na sura tofauti.
Si vibaya Manji akajua Wanayanga wengi wana uwezo wa kuongoza na wanaitaka nafasi hiyo ili naye aongeze umakini na juhudi kama ataamua kugombea tena.
Kama itakuwa wengi walipiga kelele kutaka uchaguzi. Halafu wakaamua kukaa pembeni na kujificha baada ya kupewa nafasi ya kuonyesha walichonacho kuisaidia Yanga, litakuwa ni tatizo.
Tasnia ya soka imekuwa na wapiga kelele wengi kuliko watendaji. Sitegemei kuona wanachama wa Yanga waliotaka uchaguzi kwa nguvu zote, wakikaa upande tena kimyakimya bila ya kuonyesha uzalendo wao na kugombea kama wengi wao walivyosema wanahitaji na kweli kugombea ni haki yenu.
Yanga inahitaji kuwa na Wanayanga wengi walio tayari kuisaidia. Mawazo mapya pia yatatokana na viongozi wapya wakiwemo vijana wanaoweza kwenda na wakati.
0 maoni:
Chapisha Maoni