Zidane
Zidane akitoa maelekezo kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi chake anachokinoa.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema kuwa anajivunia aina ya wachezaji alionao katika kikosi chake licha ya kutoa sare na Real Betis ya goli moja kwa moja katika mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Zidane alisema hayo baada ya kumalizika kwa mchezo huo ambao ni mchezo wake wa tatu tangu alipochukua nafasi ya kocha aliyekuwa akiinoa klabu hiyo tajiri duniani, Rafa Benitez na kueleza kuwa matokeo ambayo wamepata ni hali ya mchezo licha ya kuona kuwa walistahili kushinda.
“Tulianza vibaya na tulitambua hilo kati ya dakika ya 10 na 15 lakini mchezo ulikuwa tayari mgumu, lakini kutokana na hali ya mchezo ilivyokuwa tulistahili kupata matokeo mazuri, tulitengeneza nafasi na tulikuwa na nafasi ya kufanya vizuri,
“Naona mabadiliko kwenye kikosi chetu, ni kitu kikubwa zaidi nimekiona katika mchezo huu hadi unamalizika ni kuongezeka kwa ubora kwenye timu yetu, ni wiki yetu ya tatu na najivunia wachezaji wangu kwa walichokifanya,” alisema Zidane.
Magoli ya mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya goli moja kwa moja yalifungwa na Alvaro Cejuda kwa upande wa Real Betis katika dakika ya saba na goli la kusawazisha la Real Madrid likifungwa na Karim Benzema katika dakika ya 71 ya mchezo huo.
Baada ya matokeo hayo, Real Madrid imesalia katika nafasi ya tatu ikiwa nyuma ya Barcelona na Atletico Madrid ikiwa na alama 44 na Real Betis ikipanda nafasi moja kutoka nafasi ya 15 hadi 14 huku ikiwa na alama 22.