Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Peter Slaa akiwa na mkewe, Josephine Mushumbuzi.
DAR ES SALAAM: Wakati nyumba ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Peter Slaa ikidaiwa kuuzwa jijini Dar Desemba 27, mwaka jana, habari zinasema kiongozi huyo mashuhuri nchini na mkewe, Josephine Mushumbuzi wanakula raha mpaka basi nchini Canada. Kwa mujibu wa chanzo chetu, wawili hao wana afya njema, wanaendelea na maisha ya kila siku kama vile hakuna chochote kilichotokea Bongo kinachohusiana na wao.
Wilbrod Peter Slaa.
“Jamani nyie watu wa habari si mnasema kwamba, nyumba ya Dk. Slaa iliyopo Mbweni JKT imeuzwa? Mbona wenyewe wako huku Canada wakila maisha ile mbaya. Yaani nilivyosoma kwenye mtandao kwamba nyumba yao imeuzwa na hiki wanachokifanya hapa Canada vitu viwili tofauti. “Mimi nilitegemea watakuwa wanyonge sana. Wanafikiria kuhusu nyumba yao, lakini wala! Kwanza mnavyodhani Slaa ni mtu wa kukosa shilingi milioni 52 kweli? Jiulizeni,” kilisema chanzo hicho.
Kumekuwa na madai kuwa, benki moja jijini Dar imeiuza nyumbo hiyo iliyopo kwenye Kiwanja Na.117, Kitalu 1, Mbweni JKT Manispaa ya Kinondoni jijini Dar kwa madai kwamba, mwaka 2013 hati yake ilitumika kumdhamini mtu aliyetajwa kwa jina la Salehe ili apewe mkopo ambao marejesho yake pamoja na riba ilifikia shilingi milioni 51.5.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti moja linalochapishwa kila siku akiwa nchini humo, Dk. Slaa alisema madai ya kuuzwa kwa nyumba yake ni uzushi, kwani siyo yeye wala mkewe aliyewahi kukopa kutoka chombo chochote cha fedha na endapo kuna mtu mwenye ushahidi autoe.
Juzi, waandishi wetu walifika Mbweni kwa Dk. Slaa na kukuta walinzi waliosema wamewekwa na mfanyabiashara aliyeinunua nyumba hiyo kwa shilingi milioni 110 wakimtaja kwa jina la Ndama Hussein.
Awali, Dk. Slaa alipoondoka alidaiwa kumwacha msimamizi wa nyumba hiyo aliyetajwa kwa jina la Imma ambaye inasemekana aliondolewa Februari 2, 2016 na Kampuni ya Udalali ya Bilo Star. Dk. Slaa anayeheshimika kutokana na kuwa mwanasiasa mwadilifu na mzalendo, aliachana na uongozi ndani ya Chadema baada ya kutokubaliana na viongozi wenzake juu ya ujio wa aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa ambaye baadaye aliteuliwa kupeperusha bendera ya kuwania urais, lakini akabwagwa na mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli.
0 maoni:
Chapisha Maoni