Zahir Ally Zorro.
Risasi Jumamosi
ZAHIR Ally Zorro ni jina kubwa kwenye Muziki wa Dansi Bongo. Ameanza kutamba tangu miaka ya 1980 kwa vibao vyake vikali kama Cleopatra, Photogram na Sakina, hapa nimezungumza naye na miongoni mwa mambo aliyoyazungumzia ni hili; ‘kupiga sebene ni uvivu.’
YUKO WAPI KWA SASA?
“Sasa hivi naishi Kigamboni lakini kikazi nampiga tafu mwanangu (Banana) kwenye bendi yake ya B Band kwa kuwa na mimi najipanga kufungua rasmi bendi yangu ya Mass Media Festival. Nimeshapata vyombo na kila kitu, siku si nyingi nitaizundua.
ANAPENDA KUTUMIA ALA GANI YA MUZIKI?
“Kwa kweli chombo cha muziki ninachokipenda na ambacho nimekitumia kwa muda wa miaka 20 ni gitaa, lile ni kila kitu na tena mwanamuziki anayetumia gitaa mimi huwa namheshimu sana. Kwangu mimi huyo ndiye mwanamuziki makini.
KUNA TOFAUTI GANI NYIMBO ZAKE ZA ZAMANI NA ZA SASA?
“Kikubwa ni kwamba zamani tulikuwa tunatumia vyombo vya asili zaidi ambavyo vilikuwa vikiongeza chachu ya muziki, kipindi hiki mambo mengi yanaenda kisasa.
KITU GANI KINACHOMKERA KWA WANAMUZIKI WA BENDI?
“Naumia sana roho kuona mwanamuziki anaimba ndivyo sivyo, najua tu hakuna utulivu hapo kwenye utunzi na kitu kingine wanamuziki wanang’ang’ania sebene ambalo ndilo linawaharibu kabisa kwa sababu sebene ni uvivu wa utunzi na linadanganya unajua kuimba kumbe hakuna lolote ndiyo maana marapa wengi hawadumu.
ANAFIKIRI KWA NINI WANAMUZIKI WENGI HAWAENDELEI?
“Unajua ngoja nikwambie ili uwe mwanamuziki wa kimataifa na kuweza kupata hata kazi nje ya nchi lazima uwe ‘multipurpose’ kwa kuweza kujua kutumia kila aina ya chombo cha muziki kama gitaa, ngoma na vingine vingi, huwezi kuchuja ubora wako sasa matokeo yake ukizoea mtindo mmoja ndiyo mwanzo wa kupita kwenye meza za wateja kuomba bia.
MWANAYE MAUNDA YUKO WAPI?
“Maunda kwa sasa nilimwambia apumzike kuimba kwa sababu ana mtoto mdogo, nilipenda kwanza amlee mtoto wake vizuri sana amzoee kabisa ndiyo ataingia tena kwenye muziki kwani hata mama aliponizaa alinilea kwanza nikajitambua ndipo akaendelea na kazi.
UNAMZUNGUMZIAJE BANANA?
“Banana namuita ni mfalme wa vijana wa muziki wa live kwa sababu kama ukipata bahati ya kwenda kwenye onesho la bendi yake utaelewa ninachomaanisha kutokana na ubora wake wa sauti na vyombo anavyotumia, kwangu mimi ndiye mwanamuziki bora sana.
MWANAMUZIKI GANI ANAMKUBALI BONGO FLEVA?
“Kuna wanamuziki wengi sana nawakubali kama Snura, Lady Jaydee, Diamond na Shilole kwa kweli wanajitahidi nawaombea wazidi kusonga mbele zaidi.
HISTORIA YAKE KIFUPI
“Nilizaliwa mwaka 1954, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika Shule za Kaze Hill, Kigoma na Kisarawe, kuanzia mwaka 1964 hadi 1968.
Nilianza kujipatia umaarufu mkubwa kupitia muziki hasa nilipokuwa katika Bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mafinga ‘Wana Kimulimuli’ niliposhiriki vilivyo kuimba pamoja na kutunga nyimbo nyingi.
“Pamoja na tungo nyingi za kijamii, kadhalika nilijipatia sifa kwa kutunga na kuimba nyimbo za kuhamasisha kama vile; Mashujaa, Maneno Makini na Kadi ya Chama.
“Bendi nyingine nilizopitia ni pamoja na Super Vea (1969) ambayo makazi yake yalikuwa jijini Mwanza na Mara Jazz (1973).
“Vilevile niliwahi kuzitumikia bendi kama Mwenge Jazz Paselepa (1973), Orchestra Sambulumaa (1989), Washirika Tanzania Stars (1991), Chezimba (1996) na Mas Media Group (2002).”
About Unknown
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 maoni:
Chapisha Maoni