KOCHA MKUU WA TWIGA STARS AHIMIZA USHIRIKIANO
-Na Abubakar Khatib ‘Kisandu’, Zanzibar
Baada ya jana Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kumteuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya soka ya wanawake Twiga Stars Nasra Juma kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, leo mtandao huu umemtafuta kabla hajaelekea Tanzania bara kujiunga na kambi ya timu hiyo ambayo ilianza kambi yake hapo jana katika Hosteli za TFF zilizoko kwenye uwanja wa Karume jijini Dar-es salam.
Akizungumzia uteuzi huo huku akisisitiza ushirikiano kwa pamoja ili Twiga Stars kufanya vizuri zaidi kimataifa ambapo inakabiliwa na mashindano ya kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Zimbabwe tarehe 04/03/2016 jijini Dar-es salam na ule wa marudiano tarehe 19-20/03/2016 jijini Harare nchini Zimbabwe.
“Kwanza nimefurahi kuchaguliwa kuwa kocha Mkuu wa Twiga Stars, lakini kikubwa naomba ushirikiano kwa pamoja kwa watanzania wote, nimefanya kazi na Mkwasa na Kaijage tulishirikiana vizuri sana, sasa nawaomba watanzania tushirikiane, pia nawapongeza Idara ya Uhamiaji bila ya kuwasahau CAF, TFF na ZFA ambao wote wamenilea vizuri hao”, alisema kocha Nassra.
Nassra Juma amechukua mikoba hiyo kufuatia aliyekuwa kocha mkuu wa Twiga Stars Rogasian Kaijage kuamua kukaa pembeni.
Kabla ya Kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Nassra aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Twiga Stars tangu mwaka 2011 akimsaidia kocha Chalse Boniface Mkwasa na kipindi cha mwisho akamsaidia Rogasian Kaijage.
Nassra pia ni mwalimu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka la Wanawake (Zanzibar Soccer Queens) wakati huo huo pia ni kocha wa Women Fighter ambayo inashiriki ligi kuu soka ya Zanzibar kwa soka la wanawake, pia ni mwalimu mkuu wa timu ya Uhamiaji ya wanaume inayoshiriki ligi daraja la 2 taifa Unguja.
Nassra Juma ni miongoni mwa makocha wawili hapa Zanzibar mwenye Leseni ya juu ya ukocha wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) ambapo ana leseni ‘A’ sambamba na Hemed Suleiman Morocco kocha msaidizi wa Taifa Stars.
Kwa Tanzania nzima Nassra ni mwanamke pekee mwenye leseni ya juu ya ukocha ambayo anayo ‘A’ ya CAF na ‘B’ ya UEFA.
0 maoni:
Chapisha Maoni