YANGA imezidi kushikwa katika mbio za ubingwa baada ya leo kufungana mabao 2-2 na Prisons, huku Simba ikiifunga Mgambo Shooting mabao 5-1 na kuchupa hadi nafasi ya pili kutoka ya tatu ikiiengua Azam FC. Jumamosi Yanga ililala mabao 2-0 kutoka kwa Coastal Union ya Tanga, matokeo ambayo yaliwaumiza mashabiki wa Yanga na kujikuta wakitofautiana pointi tatu na Simba. Kutokana na matokeo ya jana, Yanga imefikisha pointi 40 ikiendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo, wakati Simba kwa ushindi huo imefikisha pointi 39 sawa na Azam, lakini Simba ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Azam ipo nyuma michezo miwili ukilinganisha na Simba na Yanga. Simba ilipata bao la kwanza dakika ya tano, mfungaji akiwa Hamisi Kiiza kwa pasi ya Jonas Mkude. Dakika ya 14, Simba ingeweza kuongeza bao, lakini penalti ya Hamisi Kiiza ilidakwa na kipa Mudathiri Hamisi. Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika ya 28, Mwinyi Kazimoto aliifungia Simba bao la pili kwa shuti kabla ya Ibrahim Ajib kufunga la tatu dakika ya 43 kutokana na kazi nzuri ya Mkude. Mashabiki wa Simba waliendelea kufurahi, baada ya Danny Lyanga kufunga bao la nne dakika ya 77 kutokana na pasi ya Said Ndemla. Dakika ya 82 Kiiza aliifungia Simba bao la tano, likiwa la 14 kwake baada ya kupokea pasi nzuri ya Hassan Ramadhan. Kiiza sasa amefungana kwa idadi ya mabao na Amis Tambwe wa Yanga, ambaye jana alifunga bao Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Wakati mashabiki wakiamini mchezo ungemalizika kwa matokeo hayo, Mgambo walipata bao la kufutia machozi dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika mfungaji akiwa Fully Maganga. Mgambo ina pointi 17 na ipo nafasi ya nane. Simba; Vincent Angban, Kessy Ramadhani, Abdi Banda, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Ibrahim Hajib/Danny Lyanga na Hija Ugando/Said Ndemla.
Mgambo JKT; Mudathir Khamis, Bakari Mtama/Bolly Shaibu, Salim Mlima, Salim Kipaga, Ramadhani Malima/Mussa Ngunda, Henry Chacha, Sunday Magoja, Mohammed Samatta, Fully Maganga, Ally Nassor na Aziz Gilla. Katika mchezo wa Mbeya, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 mfungaji akiwa Tambwe kwa kichwa kutokana na krosi ya Oscar Joshua kabla ya Juma Jeremiah kuisawazishia Prisons bao kwa kichwa dakika tano baadaye. Yanga walionekana kutaabika na uwanja uliokuwa na matope, huku Prisons ambayo imefikisha pointi 28 ikiwa nafasi ya saba ikifika mara kwa mara langoni mwa wapinzani wao. Dakika ya 62, Mohammed Mkopi aliifungia Prisons bao la pili kwa kichwa. Yanga waliendelea kushambulia kutaka kusawazisha na dakika ya 85 mwamuzi aliamuru penalti baada ya beki mmoja wa Prisons kuunawa mpira, ambapo Simon Msuva aliukwamisha mpira wavuni. Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Said Juma ‘Makapu’/Salum Telela, Deus Kaseke/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Issoufou Boubacar.
Prisons; Benno Kakolanya, Benjami Asukile, Laurian Mpalile, James Mwasota, Nurdin Chona, Jumanne Fadhil, Lambert Sadianka, Freddy Chudu/Juma Seif, Mohammed Mkopi, Jeremiah Juma na Leonce Mutalemwa/Meshack Suleiman.
0 maoni:
Chapisha Maoni