April 14, 2016 ligi ya bongo imeendelea kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja viwili tofauti, mjini Morogoro kulikuwa na mchezo kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Azam FC wakati jijini Dar es Salaam ulichezwa mchezo mwingine kati ya Yanga dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.
Macho na masikio ya wapenda soka wengi yalikuwa kwenye uwanja wa taifa ambapo mabingwa watetezi wa taji la Vodacom, Yanga imefanikiwa kupata ushindi wa magoli 2-1 kwenye mchezo huo uliokuwa mgumu na uliojaa ushindani mwingi.
Yanga walikuwa wakwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Simon Msuva dakika ya tatu kipindi cha kwanza kabla ya Kelvin Sabath kuisawazishia Mwadui FC dakika 10 baadaye akitumia vyema makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa inaongozwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
KKipindi cha pili Yanga walianza kwa kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Pato Ngonyani pamoja na Issoufour Boubacar na nafasi zao kuchukuliwa na Vicent Bosou na Godfrey Mwashiuya.
Dakika ya 71 Mwadui ilipata pigo baada ya Iddy Mobby kuoneshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa kadi nyekundu na kuwafanya mwadui wacheze wakiwa pungufu kwa dakila zote zilizosalia. Yanga walilitumia vyema pengo hilo kwa kuandika bao la pili na la ushindi dakika ya 87 likifungwa na Haruna Niyonzima.
Kabla ya goli hilo kufungwa, kuna tukio ambalo limeshangaza wengi kutokana na golikipa wa Mwadui Shabani Kado kuanguka chini lakini bado mpira ukaendelea, baada ya Kado kuona shambulizi linaelekea golini kwake akasimama na kuendelea na mchezo kisha kuruhusu bao.
Ushindi wa Yanga unaifanya kufikisha jumla ya pointi 56 pointi moja nyuma ya vinara wa ligi hiyo Simba SC lakini Simba ikiwa mbele kwa michezo mmoja. Simba ina pointi 57 ikiwa imecheza mechi 24 wakati Yanga imeshacheza mechi 23.
Mambo muhimu ya kufahamu kwenye mchezo wa Yanga vs Mwadui
- Yanga imeifunga Mwadui 2-1 kwenye mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa kwanza timu hizo kutoka sare ya kufungana magoli 2-2 kwenye mchezo uliochezwa Shinyanga.
- Simon Msuva amefunga goli lake la nane kwenye msimu huu.
- Nizar Khalfan alikuwa anacheza dhidi ya timu yake ya zamani (Yanga) huku wachezaji wengine (Jerry Tegete na Athumani Idd ‘Chuji’) waliowahi kuitumikia timu hiyo kwa misimu kadhaa iliyopita.
- Yanga na Azam zimeshinda leo ikiwa ni mechi zao za viporo vilivyotokana na timu hizo kushiriki michuano ya kimataifa na kupelekea mechi zao za ligi kusogezwa mbele.
0 maoni:
Chapisha Maoni