Jonesia Rukyaa-Mwamuzi aliyechezesha pambano la Yanga vs Simba February 20, 2016
Nimegundua
kuwa katika mpira wa miguu Tanzania mwamuzi mzuri huonekana mbaya pale
tu anaposimamia vizuri sheria za mchezo wenyewe na kuzitolea maamuzi
sahihi. Baada ya mwanadada Jonesia Rukyaa kumlamba kadi nyekundu mlinzi
wa Simba SC, Abdi Banda katika dakika ya 25 ya mchezo waliopoteza 2-0
dhidi ya mahasimu wao Yanga SC.
Lawama
zote za kupoteza mchezo ‘Wana-Simba’ wameelekeza kwa mwamuzi huyo kwa
madai kwamba alipaswa kwanza kumuonya Banda kabla hajamwonyesha kadi ya
kwanza ya manjano kwa kosa la kumchezea faulo mshambulizi wa Yanga,
Donald Ngoma. Lakini ni sababu za ‘mfa maji,’ ambaye haishi kutapatapa
wakati akiangamia.
Jonesia
alikuwa imara na alikimbia kila mpira ulipokwenda. Alifanya vizuri kumpa
kadi ya kwanza ya njano kwa Banda baada ya mchezaji huyo kumuonesha
dharau. Alijitengenezea sura ya nidhamu. Akasimamia vizuri uamuzi wake
wa kumpa kadi ya pili ya njano. Hakika mwanadada huyu ni shupavu.
Ni
mwamuzi aliyeimudu mechi na hakuwa na presha wala hakuwa muoga wa kelele
za mashabiki wa Simba. Ni bonge la mwamuzi kwa hakika, japo wengine
watapinga. Simba hawana cha kujitetea zaidi makosa yao wenyewe ndiyo
yalifungua njia za Yanga kukamilisha ushindi wao.
Simba
ilistahili kupoteza mechi ya pili mfululizo mbele ya mahasimu wao tangu
mwaka 1999. Takribani miaka 16 mfululizo iliyopita Yanga haikuwahi
kuwafunga Simba katika michezo yote miwili katika msimu mmoja wa ligi
kuu Tanzania Bara.
KADI YA PILI YA NJANO YA ABDI BANDA
Ilikuwa
ni faulo ya pili kuchezwa na Banda . Banda lilikuwa chaguo zuri sana
katika ngome ya Simba, hadi dakika 20 za kwanza Yanga haikuwa imefanya
shambulizi lolote lile la kutisha katika lango la Simba, na tayari
walikuwa wamecheza mipira mingi ya kona iliyoelekezwa langoni kwao.
Licha ya
kwamba Simba walishambulia mfululizo bila kuchoka kwa dakika zaidi ya 20
za mwanzo. Ukuta wa Yanga haukupoteza umakini wala nidhamu yao ya
mchezo. Nafikiri kwa wiki nzima kuelekea mchezo huo wa siku ya jana
Jumapili, kikosi cha kocha Mganda, Jackson Mayanja kilikuwa kimewekeza
katika mpango wa kushambulia na kuhakikisha kuwa wanapata goli la
kuongoza ndani ya dakika 15 za kwanza.
Mtogo,
Vicent Bossou alicheza na mlinzi mwingine Mnyarwanda, Mbuyu Twite kama
walinzi wa kati-namba 4-na namba 5, na mbele yao akapangwa kijana Pato
Ngonyani. Wachezaji hao watatu walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu
licha ya kupokea mashambulizi mengi. Hivyohivyo ndivyo walicheza walinzi
wa pembeni, Juma Abdul na Mwinyi Hajji.
Walitengeneza
ugumu ambao isingewezekana kwa mastraika wa Simba kupata nafasi za
wazi. Katika hali ya kaiwaida, ndani ya dakika 45 za kila kipindi cha
mchezo huwa kuna ‘vipindi vitatu,’ dakika 15 za kushambulia, dakika 15
za kupokea mashambulizi na dakika nyingine 15 za kupumzika.
Yanga
walikuwa wa kwanza kufika upande wa goli la Simba kwa jaribio la Ngoma
dakika ya kwanza tu ya mchezo, lakini mpira walipoupata Simba hakika
walikuwa na dakika 15 ngumu lakini wakastahimili presha na wakati
wakiingia katika dakika 15 za pili kwa lengo la kupumzika na kupunguza
presha ya mashambulizi ya Simba wakaanza kupiga mipira kwenda mbele kwa
kuamini uwepo wa Ngoma na Deus Kaseke na uwezo wao wa kuhifadhi mpira
ungewasaidia.
Baada ya
Banda kuoneshwa kadi ya njano ya kwanza, ambayo naweza kusema alijitakia
Yanga wakagundua kuwa nidhamu ya kimchezo ya Simba ipo chini na uwepo
wa wachezaji wao 6 wa kimataifa uliwasaidia haraka kuubadilisha mchezo
uliokuwa mgumu upande wao kuwa rahisi.
Kadi ile
ya njano ya kwanza, Banda alijitakia kwa maana alionekana kumdharau
mwamuzi wakati alipomwita, nafikiri angepewa onyo tu la kawaida kwa
kuwa ilikuwa ni faulo yake ya kwanza katika mchezo tena haikuwa ya
kutisha.
Ila
alikuwa na kiburi. Na kama angejua kilichokuwa mbele yake dakika 3
baadaye bila shaka angemnyenyekea mwamuzi wakati alipofanya faulo
isiyostahili kadi. Kadi ya pili ya manjano alipata dakika ya 25 na
ikafuata kadi nyekundu. Nini kilifuata? Aliimaliza timu yake, akamaliza
mbinu zote za Mayanja, akaondoa hali ya kujiamini katika timu yake na
mwisho wa mechi ilionekana pengo lake kwa dakika 65 liliwachosha
wenzake.
PASI MKAA YA KESSY
Katika
uchambuzi wangu kabla ya mechi nilisema kwamba Simba huwa wanakawaida ya
kupotezakupoteza sana pasi. Kwa maana fupi ni kuwa pasi zao nyingi
hupotea na niliweka wazi kuwa wataadhibiwa kwa tatizo hilo kama
hawatajirekebisha.
Licha ya
kwamba walikuwa pungufu kwa mchezaji mmoja uwanjani, Simba walijaribu
mara kadhaa kuendelea kushambulia goli la Yanga lakini wakashindwa
kuipenya ngome ngumu iliyokuwa chini ya nahodha, Bossou.
Wakati
walinzi wa Yanga walicheza kwa umakini muda wote, Hassan Kessy ambaye
alipangwa kama beki 2 wa Simba alifanya kosa la pili kubwa upande wa
timu yake. Katika mazingira yasiyotarajiwa na wengi mlinzi huyo aligeuka
upande wake na kurudisha pasi-mkaa kwa golikipa wake Mu-ivory Coast,
Vicent Angban. Pasi hiyo iliwahiwa na straika Ngoma naye akamlamba
chenga rahisi kipa huyo na kufunga goli la kuongoza upande wa timu yake.
Alichopaswa
kufanya Kessy kama hakukuwa na mazingira rahisi ya kuupeleka mpira
mbele, angeutoa tu na kuwa kona ili wajipange kuzuia. Kosa lake
lilielekea kuimaliza zaidi Simba na kuwafanya wapoteze kabisa matumaini
ya kupata ushindi.
SUB YA MWINYI KUMPISHA NOVATUS LUFUNGA
Yanga
ilipanga walinzi watano, viungo watatu na straika wawili, wakati Simba
iliwapanga viungo wanne, walinzi wanne na straika wawili. Kama kadi
nyekundu ya Banda dakika ya 25, Simba walikuwa bora katikati ya uwanja
lakini baadaye wakaanza kuzidiwa. Mzimbabwe, Justice Majabvi ilibidi
arudishwe nyuma kabisa kucheza beki ya kati sambamba na Mganda, Juuko
Murishid.
Nahodha,
Jonas Mkude akarudi chini katika kiungo namba 6 na kuwaacha Said Ndemla
na Mwinyi Kazimoto wakipanga mashambulizi. Kabla ya goli la ‘kujitakia’
walilofungwa Simba dakika ya 39, viungo wa Yanga hawakuonekana kuwa na
madhara sana lakini kitendo cha kupungua kwa mchezaji mmoja wa Simba
kiliwafanya, Kaseke, Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima kuanza kwenda
mbele.
Nilishangazwa
na mabadiliko ya kutoka kwa Kazimoto na kuingia mlinzi wa kati, Novatus
Lufunga kwa kuwa tayari Majabvi alikuwa na uwezo wa kubeba majukumu ya
beki wa kati. Kwa dakika zaidi ya 20 alicheza kama beki wa kati na
alifanya vizuri.
Nafikiri,
sub-ya kwanza ya Simba ilikuwa ni kumtoa Hamis Kizza na kuingia Brian
Majwega ambaye alikuja kupewa nafasi dakika kumi za mwisho. Uwepo wa
Mkude, Ndemla, Kazimoto na Majwega katika kiungo kungemaanisha, Ibrahim
Ajib angebaki kama mshambuliaji pekee mbele. Asingefanya lolote lakini
ingesaidia Simba kucheza vizuri licha ya kwamba walikuwa pungufu.
Majwega
ana uwezo wa kujibadilisha uwanjani na kucheza kama mshambuliaji pia ni
mchezaji ambaye angesaidia sana katika umiliki wa mpira na kuwa namba ya
ziada pia kwa safu ya kiungo. Kuendelea kumuacha uwanjani Kizza
aliyeonekana kuikamia mechi na kumtoa Kazimoto ilikuwa sub mbaya na
ilichangia kipigo cha Simba.
PATO NGONYANI, BOSSOU NA TWITE
Simba
walichukulia kutokuwepo kwa walinzi Kelvin Yondan na Nadir Haroub katika
ngome ya Yanga kungewayumbisha timu hiyo lakini alichokifanya kocha
M-holland, Hans Van der Pluijm ni kuwajaza walinzi wengi wa kati ili
kuhakikisha washambuliaji Kizza na Ajib hawapati nafasi ya kuwa peke yao
mchezoni.
Walinzi
hawa watatu wa Yanga walikuwa sababu kubwa ya ushindi wa Yanga licha ya
kwamba washambuliaji Ngoma na Tambwe walifunga magoli makali ya
kujitolea. Simba walishindwa kabisa kuupita ukuta huu wa watu watatu.
Sasa
inamaanisha katika gemu 8 zilizopita za VPL zilizowakutanisha ‘mahasimu’
Yanga SC v Simba SC, ‘Wekundu wa Msimbazi’ wamefanikiwa kushinda mechi 1
tu. Nachokumbuka kuhusu Simba ya zamani ni kwamba ilikuwa na uwezo wa
kuifunga Yanga hata pale walipokuwa pungufu uwanjani lakini Simba hii ya
sasa ikibaki pungufu tu jua imekwisha.
0 maoni:
Chapisha Maoni