Klabu ya Simba imeendelea kumkalia ‘kooni’ baki wake wa kulia Hassan Kessy licha ya kuwepo kwa taarifa kwamba alichezea kipondo kutoka kwa golikipa wake Vicent Agban baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Toto Africans uliomalizika kwa Simba kuchapwa bao 1-0 kwenye uwanja wa taifa.
Kessy ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo kufuatia kumchezea vibaya mchezaji wa Toto Edward Christopher, mara baada ya kipute hicho kumalizika Kessy alijikuta akipokea makonde kutoka kwa Agban kwa madai kuwa anatumiwa na Yanga kuharibu matokeo ya Simba.
Uongozi wa Simba leo (April 20) umekutana na waandishi wa habari ambapo umetangaza kumwongezea adhabu beki huyo kutokana na kitendo chake cha kupewa kadi nyekundu kwenye mchezo huo. Uongozi wa Simba kupitia kwa afisa habari wao Haji Manara umetangaza kumuongezea adhabu kwa kumfungia Kessy mechi tano.
“Kessy juzi ameigharimu timu hatujui kwa makusudi au bahati mbaya, Kessy ameigharimu timu kwa kucheza rafu mbaya tena yenye nia mbaya kwa Edward Christopher kwa kumpandishia mguu kichwani kwa makusudi, licha ya kuoneshwa kadi nyekundu na refa na kukosa mechi mbili, Simba inamuongezea adhabu na kumfungia mechi tano”, anasema msemaji huyo wa Simba ambayo imepoteza mechi mbili mfululizo kwenye uwanja wa taifa.
Kessy kufungiwa kwake mechi tano kunamfanya akose mechi zote za Simba zilizosalia kwenye VPL kwasababu klabu hiyo tayari imecheza mechi 25 na imebakiza mechi 5 imalize msimu wa ligi.
0 maoni:
Chapisha Maoni