‘Majogoo wa jiji’ Liverpool wameushangaza ulimwengu kwa mara nyingine tena baada ya kutoka nyuma ya Borussia Dortmund na kufanikiwa kushinda game kwenye uwanja wa Anfield kisha kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Europa League.
Kikosi cha Jurgen Klopp kilipigiliwa magoli mawili ya ‘fasta-fasta’ na kutakiwa kuhitaji kuifunga Dortmund magoli matatu ili kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo. Lakini vidume walipambana na kuupanda mlima huo kabla ya Dejan Lovren aliyetokea majeruhi na kusukuma kambani krosi ya James Milner na kuihakikishia ushindi timu yake.
Wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka 27 ya janga la ‘Hillsborough’ ambapo takribani mashabiki 96 walifariki dunia kwenye dimba la Anfield, uwanja mzima ulisimama kutoa heshima kwa mashabiki hao kwa dakika moja kabla ya game kuanza ambayo itakumbukwa vizazi na vizazi vya mashabiki wa Liverpool.
Dortmund walipata magoli mawili ndani ya dakika tisa za kwanza kupitia kwa Henrikh Mkhitaryan na Pierre-Emerick Aubameyang na kuwa mbele kwa aggregate ya magoli 3-1 baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana 1-1 kwenye mchezo wa awali uliopigwa Signal Iduna Park, Ujerumani juma lililopita.
Miamba hiyo ya Bundesliga ilipoteza nafasi nyingi za kufunga ili kuongeza gape kubwa la magoli kati yao na Liverpool kabla ya wekundu hao wa Anfield hawajarejea kwenye mchezo kwa mashambulizi ya aina yake.
Taratibu Liverpool ikaanza kurudi mchezoni kwa kutengeneza na kupoteza nafasi kadhaa. Baada ya Divock Origi kuwapa matumaini kwa kuzifungua nyavu za Dortmund dakika za mapema kipindi cha pili akiupitisha mpira katikati ya miguu ya golikipa Roman Weidenfeller, bado walidhoofishwa na goli la tatu la Marco Reus lililofungwa dakika ya 57 kwa mkwaju mkali takribani mita 14 toka golini.
Liverpool ilihitaji magoli matatu sasa ili kufuzu kwa hatua inayofuata, zikiwa zimesalia dakika 25 pambano kumalizika, Philippe Coutinho alipachika bao la pili kabla ya Mamadou Sakho kuongeza bao la tatu dakika ya 77 na kufufua matumaini ya uwezekano wa Liverpool kusonga mbele.
Alikuwa ni Lovren ambaye aliibua shangwe za mashabiki wa Liverpool dakika ya mwisho ya mchezo baada ya kupiga bao lililoipa Liverpool ushindi wa magoli 4-3 dhidi ya Dortmund na kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya Europa League.
Nguvu ya Klopp ndani ya Liverpool
Klopp alipokelewa kwa shwangwe uwanjani na mashabiki wakitambua mchango wake mkubwa ndani ya kikosi cha Dortmund kwa kufanikiwa kuchukua mataji mawili ya Bundesliga na kuifikisha klabu hiyo kwenye fainali ya michuano ya Champions League.
Muda wote wakati Liverpool inapambana kupindua matokeo, Klopp aliugeukia umati mkubwa wa Anfield na kunyoosha mikono kuwapa ishara mashabiki kuwashangilia wachezaji kwa nguvu.
Ilikuwa ni hamasa kwa mashabiki wa Liverpool ambao walianza kukata tamaa mbele ya Dortmund ambao walikuwa wametawala mchezo, lakini bado Klopp hakuacha kuwahamasisha vijana wake pia.
Matokeo hayo yamewarejesha kwenye kumbukumbu ya usiku uliopewa jina la ‘Miracle of Istanbul’ mwaka 2005 Liverpool ilipotoka nyuma kwa magoli 3-0 ya kipindi cha kwanza na kutwaa kombe la Champions League dhidi ya AC Milan.
Mechi hii haikuwa ya kuchukua kombe, lakini Klopp anaweza kuingia kwenye orodha ya makocha wa Liverpool ambao wanamajina makubwa kuwahi kukiongoza kikosi hicho kupata ushindi wa kukumbukwa.
Liverpool bado inamapungufu
Ni vigumu kukubaliana na hilo kutokana na matokeo ambayo Liverpool imeyapata usiku wa Alhamisi ya April 14 kutokana na ushapu wa safu ya ushambuliaji ambayo ilifanya kazi ya ziada kuitupa Dortmund nje ya mashindano, lakini kikosi cha Klopp kinatatizo kwenye safu yake ya ulinzi.
Sakho ambaye ni kipenzi cha mashabiki kwa sasa, alichangia goli moja kwenye ushindi huo lakini alifanya makosa ya ‘positioning’ yaliyozaa magoli yote matatu ya Dortmund.
Madhaifu ya beki wa kushoto Alberto Moreno bado yanaonesha udhaifu wa Liverpool na kumfanya Klopp kuwa na kazi ya kufanya kwenye eneo lake la ulinzi japo hakuna mtu ambaye atajali hilo baada ya ushindi wa usiku wa kukumbukwa.
Liverpool na historia ya kupindua matokeo
Ushindi dhidi ya Dortmund unaendeleza utamaduni wa muda mrefu hasa linapokuja suala la usiku wa Ulaya kwa klabu ya Liverpool.
Ushindi wa kukumbukwa utabaki kuwa ule wa 2005 wa fainali ya Champions League ambapo kikosi cha Rafael Benitez kilitoka nyuma kwa magoli 3-0 na kuchomoa yote na kupata sare ya kufungana 3-3 dhidi ya AC Milan kabla ya kushinda mchezo huo kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Mashabiki wa Liverpool mara zote huzungumzia hamasa ya Istanbul na hilo lilitokea Alhamisi usiku.
Huo siyo usiku wa Ulaya pekee wa kukumbukwa na klabu ya Liverpool, December 2004 Liverpool ilitakiwa kushinda kwa tofauti ya magoli mawili dhidi ya Olympiakos ili kufuzu hatua ya mtoano ya Champions League.
Rivaldo akaiweka mbele klabu hiyo ya Ugiriki kwa kufunga bao la kuongoza, lakini Liverpool ikapambana huku Steven Gerrard akipachika goli dakika za lala salama kuivusha klabu yake kusonga mbele kwenye michuano.
Mwaka 1977 Liverpool ilirejea Anfield kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa European Cup wakiwa nyuma kwa goli 1-0 dhidi ya St-Etienne ya Ufaransa.
Majogoo hao wa jiji walipata bao la kuongoza lakini walihitaji magoli mawili zaidi baada ya Dominique Bathenay kusawazisha bao lao. Lakini magoli ya Ray Kennedy pamoja na super-sub David Fairclough yaliihakikishia Liverpool kusonga mbele.
Mambo muhimu unayopaswa kufahamu
- Divock Origi amefunga magoli manne kwenye mechi tatu zilizopita alizoichezea Liverpool baada ya kushindwa kufunga goli kwenye mechi tisa kabla ya hizo.
- James Milner kwasasa ndiye mchezaji aliyehusika kwenye magoli mengi ya Liverpool zaidi ya mchezaji mwingine yeyote kwenye msimu wa 2025-16 (amefunga magoli 19 na assists 12)
- Liverpool haijapoteza mchezo wowote nyumbani dhidi ya timu za Ujerumani kwenye michuano ya Ulaya (W11 D3)
- Magoli yote manne ya Liverpool yalitokana na mashuti manne pekee yaliyolenga lango kwenye mchezo huo.
- Kikosi cha Klopp kimeruhusu magoli matatu kwenye uwanja wa Anfield kwa mara ya sita katika historia ya klabu kwenye michuano ya Ulaya.
- Aubameyang sasa ameifungia Borussia Dortmund magoli 37 kwenye mechi 44 za msimu huu.
0 maoni:
Chapisha Maoni