Paul Nonga alifunga goli la kwanza dakika ya 27 kipindi cha kwanza akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Juma Abdul baada ya Kigi Makasi kumfanyia madhambi Donald Ngoma nje kidogo ya box la penati.
Kigi Makasi mchezaji wa zamani wa Yanga aliisawazishia Ndanda goli hilo kwa shuti kali mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Kelvin Yondani aliifungia Yanga bao lililoipeleka Yanga moja kwa moja kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup. Kelvin alifunga bao hilo kwa penati baada ya Simon Msuva kuangushwa na Paul Ngalema kwenye eneo la penati box na mwamuzi kuamua ipigwe penati ambayo ilifungwa na Yondani.
Takwimu muhimu za mchezo wa Yanga vs Ndanda
- Paul Nonga amefunga goli lake la pili kwenye michuano ya FA, goli la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya JKT Mlale Yanga ilipopata ushindi wa goli 2-1. Paul Nonga alifunga goli la kwanza ambalo lilikuwa la kusawazisha.
- Kigi Makasi ameifunga timu yake ya zamani, Kigi aliwahi kuichezea Yanga misimu kadhaa iliyopita lakini alishindwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza na kuamua kutimkia Simba ambako pia hakudumu na kuamua kujiunga na Ndanda FC.
- Kelvin Yondani ameifunga Ndanda kwa mara ya pili kwa mkwaju wa penati, Yondani aliifunga Ndanda kwa penati kwenye mchezo wa ligi msimu huu kabla ya kuwafunga tena kwa penati kwenye mchezo wa FA hatua ya robo fainali.
- Omari Ponda na Salum Mineli ni wachezaji wawili pekee ambao ni wazaliwa wa Mtwara wanaocheza kwenye timu ya Ndanda ambayo ni ya Mtwara pia, ambao wamecheza mchezo wa robo fainali dhidi ya Yanga. Wachezaji wengine wametoka maeneo mengine ya Tanzania.
0 maoni:
Chapisha Maoni